Nilipochukua wadhifa wa kuandika waraka huu,iliniwia vigumu sana kumaliza neno moja hadi jingine. Iliniwia vigumu kumaliza sentensi moja hadi nyingine na pia kumaliza aya moja hadi nyingine. Hii ni kwakuwa,uchungu wa mapenzi ulinitesa sana. Machozi ya huzuni na simanzi hayakuacha kunitoka. Kekevu hazikucheza mbali nami. Hakika niliteseka sana. Ila namshukuru Mungu kwa maana aliniwezesha kumaliza kuandika waraka huu kwa mpenzi wangu. Aliniwezesha kukutubu sauti hii ya kilio,inayotoka ndani ya nafsi yangu.

Pascal mpenzi niliyekuenzi,angalia umeondoka. Umeondoka mapema sana. Umeondoka na kuniachia wingu. Wingu kubwa la simanzi ambalo kila uchao,linatanda na kutandazika katika anga ya maisha yangu. Sina furaha wala buraha. Karaha tu.

Simanzi,majonzi na huzuni vyote vimeitawala nafsi yangu. Tabasamu na furaha ni maneno ambayo yamekuwa adimu ndani ya maisha yangu. Yote hayo yamenitenga na kunitupa mbali kama mkongo wa ukoma. Mbali kiasi kwamba sielewi mahala nilipo. Kwa alhasili mpenzi wangu,nipo kwenye lindi kubwa la kiza. Kiza kinene cha kutisha. Najilaumu sana nafsini.

Nimegubikwa na blanketi zito la majonzi. Ninayoyaona,yanaubabia mtima wangu. Ninayoyaona,yanatangua amani ya moyo wangu. Ninayoyaona kwa sasa,yananifanya kuetuka. Moyo wangu unazuumu kufanya jambo. Jambo ambalo nafikiri litakuwa jema maana hilo ndilo indhari ya nafsi yangu.

Mpenzi wangu,ninakwina ya kumata. Nina hamu ya kuja ulipo. Nije tukae kikao,cha kuyatengeneza mambo. Nije nikuombe msamaha maana yote yaliyotendeka,mimi ndimi nilikuwa nahodha wa chombo kile. Inahalisi nije huko na ikiwezekana,tuungane pamoja kwa upendo ambao utadumu halida na halida.
                                   ***
Niitazamapo bingu,naiona ikizunguka huku ikinililia. Ninapoyatungua macho yangu na kuyaweka pembezoni,naiona dunia ikizunguka kwa kasi huku maneno USALITI yakiwa yamezagaa na kutapakaa kwenye sakafu yake kama mkeka mkubwa. Ninapoyatega masikio yangu vizuri,naisikia sauti ya nafsi yako ikilia. Inalia kilio cha huzuni. Kilio cha kite na majonzi. Kilio chako kinaniliza. Najiona sina amani kabisa. Najiona mkosaji. Najiona kama mfu anayetembea.

Kuondoka kwako kumenitia simanzi na majonzi japokuwa mimi ndimi chanzo cha yote. Maisha yangu ambayo nilidhani yatatengenea kwa kiasi kikubwa,kwa sasa yameingia doa. Kitumbua kimeingia mchanga. Tamaa zangu kanama ziliniponza. Najiona mkosaji mkubwa ambaye hata shetani hawezi kumsetiri.

Asilani sina bashasha. Uso wangu wote umesawijika kwa huzuni. Macho yangu yamevimba kama maandazi yaliyotiwa hamira. Tena mekundu mithili ya damu. Hii ni kwasababu ya kulia sana.

Mwili wangu wote umeregea. Parafujo za mwili wangu,zimeregea. Zimeregea kiasi kwamba nzi anaweza kunibwaga chini kwa kishindo ikiwa atatua mahala popote pale kwenye mwili wangu. Nimenywea na kunyong'onyea.

Maumivu yangu ya moyo yamezidi. Hayana kifani. Ni mengi sana. Haswa nikikumbuka jamala na ukarimu wako ulionionyesha pindi wabunju wangu walipofuata njia ya marahaba. Lakini mimi,mimi mpenzi,nilikuwa kinyume na ulivyotarajia. Uzuri wangu wa nje,ulikuwa sawa na ubaya wangu wa ndani. Hakika hukutambua hilo asilani.
                                   **
Wema wako na ukarimu wa moyo wako vimekuponza. Vimekuponza kiasi kwamba vimekuletea mauti. Mauti ya uchungu usioelezeka. Watu uliowaamini ikiwemo mimi, kwa njia mbalimbali,hatimaye ndio waliokupa fadhila  za punda ambazo kila siku huwa ni mateke. Wamekusaliti mpenzi. Baada ya kuona unaendelea vyema,waliamua kurudi nyuma yako. Wakaanza kukutazama kwa jicho la hasidi. Mwisho wa yote,wakauondoa uhai wako kwa tamaa za mali yako.

Tamaa ni sifa ambayo wengi wetu tumeumbiwa. Hakika nimeelewa hakuna mwanadamu anayemtakia mwanadamu mwingine mafanikio. Hilo nimejifunza toka kwangu. Japokuwa nilikupenda,lakini bado nilihisi kinyongo ndani yangu. Sikufahamu mafanikio yako,ni sawa na mafanikio yangu.

Tangu hapo awali,sikudhani kama ningeweza kufanya mambo ambayo niliyafanya. Ila baada ya kupanga mkakati wa kukuua wewe na ukafanikiwa,hapo ndipo nilijua mimi ni mnafiki na mzandiki. Nilijua mimi ni kama panya anayeuma na kuvuvia. Ila,matendo yote niliyodhani yana maana kwangu,yamegeuka na kuwa kilio kwangu. Nafsi yangu imejirudi na kunisuta. Naungulia ndani kwa ndani. Sina amani. Roho yangu,inauma.
                          ***
Kwa yote niliyopitia baada ya kifo chako,nimejifunza mengi. Nimejifunza kwamba,kweli nafsi haifi bali mwili. Ujapouua mwili,nafsi itabaki. Nafsi yako inanisuta kila uchao. Kila niyafumbapo macho yangu,nakuona. Nakuona ukiwa unalia. Unalia kilio cha huzuni. Machozi yako hubadilika kila uchao na kuwa damu. Mara nyingine nakuona ukinihukumu. Mara nyingine nakuona ukinijia huku ukiwa na tabu kubwa lilioandikwa USALITI. Hakika najutia kosa langu mpenzi. Naomba unisamehe popote ulipo. Sikukusudia kukutenda ila,tamaa ya mwili wangu,iliyochochewa na misemo ya marafiki zangu,ilinifanya nikunyamazishe. Sikujua kwamba mali huisha. Sikujua kwamba,utajiri wa duniani ni kama maji ya moto. Hayo yote sikujua mpenzi,hadi pale yale yaliyonifika yaliponifika.

Sipendi kukumbuka kwamba,safari yako ya maisha,ilifupishwa ghafla. Sipendi kukumbuka  kwamba,mimi nilikuwa kati ya papa na papaupanga waliohakiki chombo chako ulichokuwa ukisafiria baharini hakifiki nchi kavu. Sipendi kukumbuka kwamba,mitego yote tuliyokuwekea,hatimaye ilikunasa mpenzi wangu.

Baada ya taarifa za tanzia kutufikia,tulifurahi sana. Tulijiona kama panya aliyeondokewa na paka. Kumbe furaha ya siku ile,ndiyo ilikuwa ya mwisho ndani ya maisha yangu. Laiti ningelitambua hilo,mipango yote tuliyoipanga,ningeitangua. Lakini haikuwa hivyo,yamemwaika mpenzi. Hakika ni muhali kuzoleka. Nateseka.

Nilipouona mwili wako ulivyokuwa umefanywa kinyama,hakika sikuamini macho yangu. Nilitamani iwe ndoto ya kutisha. Ili niamkapo,niwasimulie walimwengu. Kumbe haikuwa hivyo. Ilikuwa mubashara.

kichwa chako kilikuwa kimetenganishwa na mwili wako,hakika nilishtuka sana. Machozi mengi yalinitoka. Nilijilaumu nafsini. Roho yangu iliniuma. Sauti yako niliisikia masikioni mwangu. Ilikuwa ni sauti ya upole. Sauti iliyojaa mapenzi ya dhati. Sauti ya kutuliza chote kilicho na mashaka. Ulinambia,'mpenzi,nimeenda ila,naomba uwaambie walimwengu ukweli. Waweze kuelewa siri ya kifo changu. Nakupenda sana mpenzi wangu,japo umehusika na kifo changu.' Kila niyakumbukapo maneno yako hayo,huwa nashindwa kuyazuia machozi yangu.
                            
Tabasamu lako la uraufu,uzuri wako wa sura,wema wako,ukarimu na utendeti wako wa mambo,vyote umefifia navyo. Ndoto zako na malengo yako ambayo ulikuwa karibu kuyatimiza,umeondoka nayo.

Hapa nilipo,nimebaki na picha yako tu. Picha ambayo nikiitazama,machozi hayeshi kunidondoka. Picha ambayo nikiitazama,nakumbuka mema uliyonitendea. Picha ambayo nikiitazama,nakumbuka mengi sana tuliyoahidiana. Nilikusihi usije kunisaliti. Jibu lako lilinishtua sana. Kumbe ulikuwa unasema kile ambacho kingetokea katika maisha yako. 'Mpenzi,mimi siwezi kukusaliti. Nakupenda sana na kukuheshimu. Nimekupa mtima wangu. Nimekupa kila kitu changu. Kiweke salama maana yote hayo,yatakuwa idhibati tosha kwa yule atakaye jaribu kuingia ndani ya ulingo wetu wa huba. Nakuomba ukae kando na marafiki wabaya. Maana hao ndio watakaokuchochea kufanya hivi au vile. Na mwisho wa yote,watakucheka na kukutoroka. Ubaki peke yako ukisaga meno na kujilaumu.' Maneno yako hayo ndiyo sasa nayaelewa. Sina jinsi. Yalitendeka yaliyotendeka. Ndio maana nipo hapa kuomba msamaha.
                                     ***
Majonzi na simanzi vyote vimenikumbatia. Ninalia kilio cha kite na simanzi. Barua yangu kwako,itakuwa ndefu na ya kuchosha ikiwa nitakutubu yote mazuri uliyonitendea. Hakika sitosahau ulivyojituma kunisomesha hadi chuo kikuu. Mengi sana nakukumbuka kwayo ila,naomba niibwage kalamu yangu chini. Nimezidiwa mpenzi. Moyo wangu unaniuma. Siwezi kuendelea kuandika ila ningependa ujue kwamba moyo wangu unakupenda na una hamu ya kukuona tena. Kwa yote niliyokutendea,naomba samahani. Najua mahala ulipo,utanisamehe. Ukifanya hivyo,furaha itarudi ndani ya maisha yangu. Nakupenda sana Pascal wangu. Nakupenda sana.

                      ***MWISHO***


WhatsApp Google Map

Safety and Abuse Reporting

Thanks for being awesome!

We appreciate you contacting us. Our support will get back in touch with you soon!

Have a great day!

Are you sure you want to report abuse against this website?

Please note that your query will be processed only if we find it relevant. Rest all requests will be ignored. If you need help with the website, please login to your dashboard and connect to support