Ubakaji ni tendo la kumlazimisha mtu afanye asichokikubali ndani ya nafsi yake. Mara nyingi,linatumika kuhusu ngono isiyo na hiari kwa mtu. Ingawa unyama huu,aghalabu hufanyika dhidi ya wanawake,ila napenda kusema pia watoto wa kiume hufanyiwa bali na watoto walio na akili punguani wasioelewa kinachoendelea.
Ubakaji unaweza kutumia nguvu za mwili, mamlaka aliyo nayo mtu katika mazingira fulani au kwa kutumia vitisho.
Wale ambao hufanya tendo hili la kinyama,ambalo ni kinyume na sheria na linaorodheshwe kama kosa la jinai,ni wale ambao wana tamaa ya kupitiliza hivi kwamba,wanashindwa kabisa kuzuia mtafaruku wa kihisia ndani ya mwli wao. Baada ya kushindwa kuzuia hisia na ashiki zao za mwili,basi huishia kufanya tendo hili ambalo baada ya kumaliza,unajirudi na nafsi yako inakuhukumu kwanini ulitenda.
Kwa kawaida,nwanadamu huongozwa na nguvu fulani. Nguvu hizo,za uwili,ndizo humfanya mtu kutenda wema au ubaya. Na mara nyingi,ukiamua kutenda jambo ambalo ni kinyume,huwa kuna nguvu ambazo hujibizana ndani ya nafsi yako. Nguvu za uzuri na nguvu za ubaya. Lakini mwanadamu kwakuwa hapendi kushindwa,basi huamua kufuata nguvu hasi,nguvu za ubaya ili kutimiza kile ambacho mwili umetamani. Iwapo mwanadamu atashinda vita vya nafsi yake,na kufuata nguvu chanya,nguvu za uzuri,basi mambo kama haya yasingewahi kusikika wala kujulikana yapo na pia,maneno haya ninayoyaandika,yasingelikuwepo. Ila kwakuwa kwa sasa yapo,basi lazima niyaandike.
Ubakaji ni tukio baya sana kwa nafsi ya mtendaji na mtendewa. Kwanza,mtenda hujirudi na nafsi yake humuhukumu. Hapo ndipo mambo huwa mabaya sana maana saikolojia yake,huathirika vibaya na mwisho wa yote,akili yake huweza kuharibika na kuishia kuwa taahira,zezeta asiyejua be wala te!
Pia kwa muathirika,tukio hili laweza kuathiri pakubwa afya yake au kuathiri maisha yake yote kwa ujumla mama sio kusababisha kifo haswa pale anapofanyiwa tendo hilo na watu wengi kwa ujumla.
Kwakuwa sheria ina mkono mrefu,watendaji wa mambo kama haya hujipata kwenye mikono ya serikali na kuhukumiwa kifungo cha maisha kama sio cha kunyongwa. Wengine ambao hutenda mambo haya,huepuka mkono wa sheria kwa kuzunguka mbuyu. Wengine hutoroka na kwenda kusikojulikana. Wengine kama akina jadi kubeli ambao wamejigmhusisha na mambo kama haya,hufanya mpango wa kumpandikizia mtu dhambi hiyo kwa kumlipa pesa nyingi. Hivyo yeye atakuwa amejiondoa kwenye anga hizo na wewe ukawa ndiwe mshtakiwa japokuwa kwa hali halisi,wewe siwe uliyehusika.
Hili hutokea iwapo,anayepandikizwa,anatoka katika tabaka la kimaskini. Umaskini ni mbaya mama. Umaskini unaweza kufanya mtu kufanya mambo ambayo kamwe hakutarajia almuradi tu,aweze kupata pesa za kujikimu kimaisha. Na hili ndilo kwangu lililonitokea. Sio kwamba mama nilibaka la,siwezi kamwe kuishusha hadhi ya familia yetu na wala kwenda kinyume na maneno yako mama ambayo ulikuwa ukiniasa.
Baada ya kutoka nyumbani,umasikini ulinilemea sana. Kila nilililokuwa nikilifanya,halikuwa linafanikiwa. Hakika,nililia sana. Nilijiona kama ambaye nikiyeumbwa kubeba umaskini wa watu wengine. Madhila niliyoyapitia,kunyanyaswa na kupokwa pesa zangu za mshahara kwa kusingiziwa,kulinifanya nione dunia chungu. Kulinifanya nilie sana. Sikuwa na jinsi bali kukubali hali halisi ya maisha yangu japokuwa maisha yalikuwa machungu sana kwangu.
Nilikumbuka maneno yako. Nikaamua kuyafanyia kazi. Kusali na kusoma neno,yote niliyatenda bila mafanikio. Nilijisaili sana. Maswali ambayo sikuwa na majibu. Mungu yu wapi? Je,wanadamu waliumbwa ili kuteseka? Au kuna wale ambao waliumbwa kuwa zaidi ya wengine? Mungu ni mbaguzi au? Au Mungu wetu huhongwa ili kumpa mtu maisha mazuri? Yalikuwa baadhi ya maswali kati ya mengi ambayo yalinighashi kila uchao ndani ya anga ya fikra zangu. Lakini kuna kile kilinifanya nitambue kwanini wapo matajiri na wapo walio masikini,Ezi! Niliamua kuishi maisha hayo ya kuteseka mpaka pale nafasi ya kuyabadili maisha yangu ilipofika,nikaamua kuchukua hatua nyingine. Hatua ya maisha. Hatua ambayo itawanufaisha wengine,wala sio mimi. Niliamua kufanya haya mama,ilmradi tu,niweze kutimiza ahadi yangu kwako. Sikupenda kufa kabla ya kutimiza ahadi yangu kwako.
**
Barua yako mama,uliyonitumia siku si nyingi,iliniiifungua milizamu ya macho yangu na mvua ya machozi ikaanza kunibubujika. Japokuwa nilijikaza kiume lakini tone moja tu la chozi,likilotoka kwenye jicho la shimali,ndilo ambalo lilichangia mimi kufanya haya na ndiyo maana nakuandikia waraka huu wa huzuni na furaha kwa upande mwingine. Najua kwamba,utakapoipokea barua hii,kiviga cha kuashiria mwisho wa safari yangu,kitakuwa kimetanda kotekote. Utakapo ipokea barua hii,nakuomba uwe mtulivu na kushukuru Mungu maana kile chote kifanyikacho,hufanyika kwa sababu kuu. Mtu kufa,sio kwamba amekufa la,mtu hufa ili kuupisha uhai mwingine kuja duniani. Ndo haya sasa yafanyikayo kwangu.
Ujumbe wako,katika aya ya pili mstari wa sita kwenye barua yako,ndio ulichangia mimi kutoisoma barua yako na kumbukumbu ya mambo mengi ambayo nilikuahidi ikanijia. Naomba samahani mama kwa kosa langu la kukawia bila kurudi nyumbani. Ila wanasema mkono mtupu haurambwi. Na ndiyo maana mimi sikutaka kuja. Najua wengi walidhani nimepata ulwa,nafaidi utamu wa tamu tamu mahoda ila sio hivyo. Maisha mama maisha. Maisha yalichangia. Mazingira ya maisha yangu,hayakuwa yakitazamika. Kila uchao,msimu ulibadilika. Ukija msimu wa masika,kesho huja kiangazi. Ukitoka kiangazi,huja kipupwe chenye baridi kali. Maisha yangu yalikuwa ya mzunguko ambao baada ya kuuzunguka,unaishia kurudi pale pale. Lakini sikukata tamaa.
Manrno yako yaliyopigiwa mstari kwenye barua yako,yalinifanya nimkumbuke sana baba. Baba alikuwa ni mtu wa kujituma sana hadi pale mauti yalipomfika baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa ambao hatukujua ni upi kutikana na hali yetu ya kimaisha. Majirani walitucheka sana na wale waliokuwa wakijidai kwamba ni wacha Mungu na marafiki,waliamua yao. Wakatutenga kama wakongo wa ungonjwa wa ukoma.
Jamaa wa ukoo wetu nao walitukimbia. Nakumbuka maneno ya mjomba. 'Wafao na wafe' Kamwe sitoyasahau. Nadhani umaskini wetu ndio uliwafanya wengi kututoroka. Tulijikaza kisabuni. Mimi nilijitolea kujenga jeneza la mbao za mbavu za mbwa. Na mwishowe tukamlaza baba na kumfukia kwenye kaburi ambalo mimi na dada yangu Shamimu tulilichimba. Huo ukawa mwisho wa baba yetu tuliyempenda kwa dhati.
Baada ya baba kulazwa kwenye nyumba yake ya milele,Shamimu,dada yangu aliamua kwenda mjini kutafuta maisha. Kule mjini,aliweza kupata tabu sana. Kulingana na jinsi alivyonieleza,aliteswa sana kazini alikokuwa kama kijakazi. Mama mwenye nyumba,alimnyima chakula. Pesa,hakuwa akimpa. Kila mara alilaghai kwa singizio kwamba dada kakosa hiki ama kile. Hadithi ya maisha yake ilinitoa machozi. Natumai baada ya barua hii,maisha yenu yatabadilika kwa asilimia kubwa mama. Nimeamua kutoa kafara,ili maisja yenu yawe safi. Ahadi yangu mama,niitimize.
Nakumbuka mama uliteseka sana. Kazi za sulubu na za kijungujiko ulizifanya ili tupate kula. Mwili wako uliregea sana. Ukawa kama utumbo wa nswi. Japokuwa ndizo zilitusetiri kimaisha,iliniuma sana mama. Sikupenda kuona ukiteseka. Sikupenda kuuona ukiunia. Ukisadiki ulikuwa unafanya kazi kwa hata kwa mvua. Hata ndala wala makubadhi,hukuwa. Uliumia sana. Jasho lako,lilikuwa la gharama kwetu. Jasho lako,lilikuwa kama ndilo Mungu wetu lakini mwishowe ulilemewa mama. Gonjwa baya lilikusakama. Likakuacha si wa uhai si wa ufu. Si wa maji si wa uji. Ulikonda sana mama. Sitaki kukumbuka,maana kila nikumbukapo...
Elimu hukutunyima. Ulijikaza kisabuni. Uliamuni kwamba,elimu,itatutoa siku moja kwenye lindi tulikokuwemo la ukata na ufukara wa sina sinani tukiulizwa,hatuungami. Nakumbuka kauli yako,'elimu ndio ufunguo wa maisha' kauli yako ilikuwa ya kutia moyo ila kadri siku zilivyozidi kusonga,hata kusoma kwenyewe kulitushinda. Nashkuru kwa ulivyojitolea na ndiyo maana nimeamua kulipa fadhila zangu kwako kwa hili,japo litauma ila kubali jinsi yalivyo.
Naamini kama baba angelikuwa hai,haya yote tungeyaona kwenye magazeti au kuyasiki ila ndo hivyo. Dunia ikiamua kutupoka. Ikatunyang'anya tonge letu mdomoni. Baada ya baba kuiaga dunia na kwrnda kwa baba ni lillahi inna illahi rajiuna,ndipo nilifahamu,chema hakidumu kamwe.
Nayakumbuka mengi. Nakumbuka ulivyowavumilia majirani waliokuwa wakitusimanga na kutusindikiza kwa matusi ya kila nui. Nakumbuka yule mjumbe bwana Dingi,alivyokupoka kipande cha shamba kwa kusingizia yeye ndiye mmiliki. Uliamia kumwachia kwa moyo safi. Sauti yako kwa wakati huo,ilikuwa changa. Changa hivi kwamba,haikuwa na uzito wa kusikika. Maana hata wale waliokuwa karibu,walijipalia makaa. Wakageuka kitatange na wengine panya,anayeuma na kuvuvia.
Ni dhahiri dau la mnyonge haliendi joshi. Hilo naliafiki na kukubaliana nalo. Maana maisha ambayo tuliishi na maisha ambayo nimeishi,nimejifunza mengi sana. Mengi ambayo nikiyaandika,yatakuwa ya kuliza kila mwanadamu ambaye ataupitia ujumbe wenyewe. Sitaki wengi wajawe na hisia. Walie na wengine kufa kutokana na hisia na kunisingizia mimi ndimi chanzo cha kifo chao. Hapana.
Hata kama tulikuwa masikini wa sina sinani, wakata waliokuwa wakipigiwa mfano bado ulikuwa mama. Mama uliyeonyesha mapenzi kwa wanao wawili. Hata tashbihi nyingi shuleni zilizokuwa zikitumika kulinganua umaskini,walitumia aila yetu. Wengi wa wanagenzi walipenda sana kutoa mfano na umasikini wetu. 'Wachochole kama familia ya kina mwafulani' ulikuwa kibwagizo cha kila sentensi waliyokuwa wakitema wanafunzi wenzangu. Nililia sana ila ulinipa moyo. Nasema wewe ulikuwa mama wa kipekee,ambaye ulijitolea juu chini kuhakiki sisi wanao tunaishi tu. Wema wako mama,siwezi kuumaliza kuuelezea. Hata kama nikiueleza wema wako,wengine watauona kama ubaya. Si wajua binadamu?
Sina haja ya kukumbusha uliyoyafanya. Najua wajua yote uliyoyafanya. Ikiwa nitaamua kuandika wema na uzuri wako kwenye barua hii ndogo,wakati wangu utaisha na hutoipokea barua hii ninayoiandika. Barua hii ni ya siri yangu. Siri ya maisha yangu. Siri ya kuamua kufanya haya niliyoyafanya. Nilitamani nikae na siri yangu hadi siku ya kufa ila nimeamua tu kukwambia iki uweze kufahamu hali halisi ya maisha. Ufahamu kwamba umaskini ni kitu duni sana kwenue maisha ya mwanadamu,na unaweza kukufanya utende mambo ambayo hukutaraji.
Siri hii,sitoitoa moja kwa moja. Najua akili yako bado ipo razini. Na ikiwa upo makini,najua ushajua siri ya maisha yangu. Nikukumbushe labda,siri yangu ipo kwenye aya ya nane ya barua hii. Hilo tendo ndilo lililonipata mimi mama. Sikuwa na jinsi. Niliamua ili kutimiza ahadi yangu kwako. Sikuwa na namna nyingine mama. Maisha yalivyokuwa yakinipekeleka,niliamini nitakufa kabla sijatimiza ahadi. Kila siku wanasema ahadi ni deni na dawa yake ni kulipa. Ninalipa kwa hili mama.
***
Mkono wa kushoto ndio unaokutubu barua hii,niatakayoituma kwako kupitia dada yangu,mwanao Shamimu. Baada ya kukuaga na kwenda mjini kutafuta mali,ndipo nilioopatana na dada yangu. Kwa mara ya mwanza sikumjua ila kwakuwa wanasema damu nzito kuliko maji,tulijuana. Hali niliyompata nayo,iliashiria anakwenda kutuacha. Mwili wake,ulikuwa umenyong'onyea na kukondeana mithili ya kimbaumbau mwiku wa pilau.
Sikumuacha. Niliamua kukaa naye kwa maisha niliyokuwa nikiishi mimi. Nilimfanyia kila jambo. Hali yake ilipokuwa mbaya,nilimpeleka hosipitalini. Nilijituma sana ili kumuauni dada yangu. Cha kushukuru,hali yake ilirejea. Alipata afua japo kidogo. Sasa hivi,utakapo mwona,hutoamini. Ni mzima kama ngarange za mvule.
Nilikuahidi kwamba,ipo siku nitayabadilisha maisha yako kwa hali yoyote ile. Najua pindi utakapoipokea barua hii,maisha yenu yatakuwa yamebadilika vya kutosha. Huzuni yako iliyojaa moyoni mwako,inaenda kuyeyuka muda si mrefu. Hata lile banguzi lililogandama ndani ya moyo wako,linakwenda kupona.
Mustakabali wa maisha yenu,wewe na dada nimeshaujenga. Ningependa umrejeshe shuleni aweze kuendelea na masomo yake. Naamini kwa sasa masomo hayatomkataa kama hapo awali. Uhakiki anasoma kwa bidii ili aweze kutimiza lile lengo lake la kuwa daktari. Nahitaji asome ili naye aweze kuitunza familia yake kama atabahatika kupata.
Hapa nilipo,najua dunia sio mbaya. Walimwengu ndio wabaya. Haya yote yasingetupata ikiwa wanadamu wangekuwa wema kwetu kama baba alivyokuwa kwao enzi zile. Mungu ndiye mkuu kwenye maisha. Na kudura zake kamwe haziwezi kuondolewa na jitihada za mwanadamu. Akipanga hili au lile,lazima litimie. Na naamini yeye ndiye alipanga pia hili langu. Mama,hakuna jaribio la kudumu,hilo elewa na pia ufahamu kwamba,kila kilicho na mwanzo lazima kiwe na mwisho. Mwisho wa kutaabika kwenu umefika. Mungu aliweza kusikia kile kilio chako na kufungua milango. Milango ya baraka ya uchungu. Naomba zawadi hii pokea. Tena ipokee kwa mikono yako miwili. Mungu anaelewa maisha ya mwanadamu. Jinsi yatakavyo anza na yatakavyo malizika.
Dada anakuja nyumbani kukuchukua na akupeleka mahala pazuri nilipopanunua na kukujengea baada ya kuamua hili. Pia,pesa zingine nilizoziweka kwenye akaunti yangu,mtakwenda kuzitoa kwa kufuaata taratibu zote utakazoelezwa na benki husika.
Mama,sina budi kukuaga. Safari yangu ya kwenda imeshafika. Pingu zilizokuwa mikononi mwangu,zishafunguliwa. Safari ya kifo changu,imekaribia. Wanasema hakuna mwanadamu anayejua siku yake ya kufa,ila rekodi nimeshavunja. Nafa nikiona mama.
Dakika zisizopungua ishirini,nitakuwa maiti. Maiti ya kunyongwa kutokana na kosa la ubakaji. Ubakaji ambao sikutenda japo umasikini ulinifanya niamue nililoamua. Nilikabidhiwa kesi hii na tajiri mmoja aliyesafiri kwenda nchini Marekani baada ya kunilipa pesa nyingi sana ambazo ndizo nilizitumia kutimiza ahadi yangu.
Nasema ahsante mama kwa kujitolea kwako katika malezi. Nawatakieni maisha mema. Maisha ya furaha na upendo. Maisha yaso kinyongo. Maisha ya kuwatunza na kuwajali wengine. Kulipiza baya kwa baya sio busara mama. Kuwa kielelezo bora katika jamii na ninaamini,maisha yenu yatakuwa bomba. Kwakuwa dini yetu inaamini kuna uhai baada ya mtu kufa,niseme ipo siku tutaonana hata kama jehanamu au peponi.
Kwaheri mama. Kwaheri Shamimu. Kwaheri dunia. Wote kwaherini...
END